Utu ni sifa mojawapo muhimu katika mahusiano mazuri maishani mwa binadamu. Utu huhusisha wema. Utu ni sifa ambayo huhusishwa na wahusika mbalimbali katika dunia halisi na hata kwenye dunia ya fasihi. Wahusika ni muhimu katika fasihi kwa vile kupitia kwao, mwandishi huweza kupitisha ujumbe aliokusudia kwa wasomaji. Wahusika huwa wa aina mbalimbali wakiwemo wahusika wa kiuhalisiajabu ambao pia huchangia katika kupitisha ujumbe wa mwandishi sawia na wahusika wa kihalisia. Tafiti za awali zimewasawiri wahusika binadamu wakionyesha utu kwa sababu ni sifa muhimu anayopaswa kuwa nayo binadamu. Hata hivyo, waandishi wa Kiswahili akiwemo Said A. Mohamed wamesawiri wahusika wa kiuhalisiajabu wakionyesha utu kwa viumbe wengine. Huu ni mtindo ambao umeanza kutumiwa katika riwaya mpya na waandishi wa fasihi ya Kiswahili. Hivyo basi, utafiti huu ulichanganua kiuhakikifu wahusika viumbe wa kiuhalisiajabu katika riwaya teule za Said A. Mohamed ili kudhihirisha kwamba hata viumbe wasio binadamu huwa na sifa ya kibinadamu ya utu. Lengo mahususi lililoongoza utafiti huu lilikuwa kufafanua jinsi viumbe wa kiuhalisiajabu wanavyodhihirisha utu katika riwaya za Said A. Mohamed. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya kiuhalisiajabu kama inavyofafanuliwa na Zamora na Wendy (1995). Nadharia hii hueleza matukio katika hali ya kutisha, kushangaza na kuogofya kwa kuziwasilisha kana kwamba ni hali ya kawaida. Eneo la utafiti likiwa fasihi ya Kiswahili, utanzu wa Riwaya. Sampuli ya kimakusudi ilitumika kuteua riwaya tatu za Said A. Mohamed hususan: Babu Alipofufuka (2001), Dunia Yao (2006) na Nyuso za Mwanamke (2010). Data ilikusanywa kutokana na kusoma riwaya hizo tatu zilizoteuliwa na kudondoa sehemu zinazolingana na lengo la utafiti. Data ilidondolewa, ikanukuliwa, ikapangwa kisha kuchanganuliwa. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa kwa kweli viumbe wa kiuhalisiajabu wana sifa za utu kama upendo, ukarimu, kusamehe miongoni mwa mengine.