Muhtasari Uwezo wa wanyama pori walao mimea kudhibiti uvamizi wa mimea ya kigeni bado ni swali kuu katika ikolojia. Kuna ushahidi kwamba wanyama pori walao mimea wana uwezo wa kuzuia uvamizi wa mimea ya kigeni, lakini haijulikani iwapo inafanyika na jinsi inavyofanyika kwa ujumla katika mifumo ya ikolojia yenye aina mbalimbali ya wanyama pori na vikundi vitendakazi vya mimea, hasa kwa muda mrefu (wa muongo).Kwa kutumia data kutoka kwa majaribio matatu ya muda mrefu (miaka 13 hadi 26) yaliyomo Kenya ya kati, tulipima athari za wanyama pori kwenye wiani wa cactus vamizi za kigeni, Opuntia stricta na O. ficus‐indica (kwa pamoja, Opuntia), ambazo ni miongoni mwa spishi vamizi zaidi duniani. Pia tulichunguza uhusiano kati ya utajiri wa aina za wanyama pori na uwezekano wa kutokea kwa O. stricta katika kiwango kikubwa cha mazingira (6150 km2).Wiani wa Opuntia ulipunguka kwa kati ya 74% na 99% katika takriban viwanja vyote vinavyofikiwa na wanyama pori walao mimea na uliongezeka kwa kasi zaidi katika viwanja ambavyo havijumuishi wanyama pori walao mimea. Athari hizi zilichangiwa kwa kiasi kikubwa na wanyama walao mimea ambao ni wakubwa sana (≥1000 kg), hasa tembo.Katika kiwango kikubwa cha mazingira, uwezekano wa kutokea kwa Opuntia uliwiana hasi na makadirio ya utajiri wa aina za wanyama pori walao mimea na uwezekano wa kutokea kwa tembo. Kwa wastani, uwezekano wa kutokea kwa Opuntia stricta ulipungua kutoka ~0.56 hadi ~0.45 kwani utajiri wa aina za wanyama pori walao mimea uliongezeka kutoka spishi 6 hadi 10 na ulipungua kutoka ~0.57 hadi ~0.40 kwani uwezekano wa kutokea kwa tembo uliongezeka kutoka ~0.41 hadi ~0.84. Matokeo haya ya viwango mbalimbali yanapendekeza kwamba athari zozote za uwezeshaji wa Opuntia na wanyama wa pori walao mimea (k.m. utawanyishaji wa mbegu/mimea) huzidiwa na ukandamizaji (k.m. kuliwa, kung'olewa, kukanyagwa).Usanisi. Matokeo ya majaribio na uchunguzi wetu kwamba wanyama pori hudhibiti uvamizi wa cactus za kigeni yanachangia ushahidi kwamba kuhifadhi na kurejesha mikusanyiko ya wanyama walao mimea wa asili (hasa wale wakubwa sana) kunaweza kuongeza udhibiti wa jumuiya ya kibayologia dhidi ya uvamizi wa mimea. [ABSTRACT FROM AUTHOR]