Muhtasari: Shughuli za kibinadamu zinaweza kuwa na athari kubwa kwa wanyamapori. Athari hizi huweza kutofautiana kutokana na aina ya shughuli na tabia ya wanyamapori husika. Ingawa athari za kitabia zimetafitiwa vizuri, tafiti katika utimamu wa mwili na fiziolojia ni chache hasa katika spishi zinazoishi katika makundi.Tulifanya majaribio kuchunguza athari za ufugaji wa kila siku katika ukuaji wa watoto na athari za mkazo kwa idadi ya fisi madoa doa huru katika eneo la Kreta ya Ngorongoro kwa kipindi cha miaka 24.Ufugaji katika eneo la Kreta ulidhibitiwa kuwa katika mipaka ya koo mbili tu kati ya nane za kitafiti, hivyo kuturuhusu kulinganisha ukuaji wa watoto kati ya koo ambazo ufugaji ulifikia na zile ambazo ufugaji haukuathiri. Vile vile, tulilinganisha kiwango cha metabolite ya glukokotikoidi katika kinyeshi (fGMC), ambacho ni kiashiria cha mkazo kwa wanyama kati ya koo zilizofikiwa na ufugaji na zile ambazo hazikufikiwa kwa kutumia sampuli 975 za kinyesi kutoka kwa fisi madoa 475.Hatukupata tofauti ya wazi katika ukuaji wa watoto na mkazo kati ya koo zilizofikiwa na zile ambazo hazikufikiwa na ufugaji kuonyesha kuwa ufugaji haukuwa na athari hasi kwa fisi madoa. Kukosekana kwa athari hasi pengine kunatokana na athari mjumuiko za asili ya ufugaji kunakotabirika na usio na usumbufu, ikilojia‐jamii ya fisi madoa na uthabiti wa idadi kubwa ya mawindo ndani ya Kreta.Matokeo ya utafiti wetu unaonesha kuwa, shughuli za kibinadamu zinaweza kuendana na kustahilimiliwa na aina fulani ya spishi zinazoishi katika makundi, hasa ikiwa muingiliano kati ya spishi na shughuli utadhibitiwa. Kwa hivyo, utafiti wetu unatoa mitizamo mipya kwa wana ikolojia, wana biolojia wa uhifadhi na washikadau katika kutathmini migogoro ya binadamu na wanyama na kuleta usawa kati ya mahitaji ya jamii za wanadamu na wanyamapori. [ABSTRACT FROM AUTHOR]